Kenya Socialist Web Site
Kuanzisha Chama cha Wafanyikazi cha Kenya
(CCW)
Utangulizi
Chama
Mchango wangu wa mapambano
Ni kiasi tu
Ninachoweza kukifanya
Bali mapambano
Si yangu peke yangu
Wala mapinduzi
Hayawezi kufanywa na mtu mmoja
Kwani mapambano
Ni yetu sote
Na mapinduzi
Yataletwa na juhudi kubwa
Za pamoja
Za wewe na mimi
Na wote
Tunaopigania maisha bora katika jamii
Na wewe na mimi
Na wengine
Kama sisi
Tukiunganishwa
Na kushikamanishwa
Na msimamo mmoja wa kisiasa
Itikadi na adili moja ya kimapinduzi
Nidhamu ya kutuoganaizi pamoja
Lengo moja la kupigania ukomunisti
Nia moja ya kujitoa kupambana
Pasina kurudi nyuma ama kukata tamaa
Tunaitwa chama
Chama cha mapinduzi
Na tukiwa wanachama
Katika chama
Chama cha mapinduzi
Tutapiga hatua nyingi mbele
Katika safari ya ukombozi wa jamii yetu
Tutaweza kuyafanya mapinduzi yakafanyika
Pasina kuwa na chama, chama cha mapinduzi
Chama cha nadharia na itikadi ya kikomunisti
Hapawezi kufanyika mapinduzi ya usoshalisti
Ndiyo, popote tulipo wazalendo na wanamapinduzi
Sharti tuwe kwa chama, chama cha mapinduzi
Chama cha kikomunisti
Kwani mwanamapinduzi huunda chama
Nacho chama huunda wanamapinduzi
Na wanamapinduzi hufanya mapinduzi
Mwanamapinduzi
Asiekuwa kwa chama, chama cha mapinduzi
Asiefanya kazi
Ya kuunda na kujenga chama ikiwa hakiko
Huyo si mwanamapinduzi
Ni msabili
Au pengine ni msomi wa mapinduzi
Asiekuwa kwa chama
Asieshiriki kwa kazi ya kuunda chama
Si mwanamapinduzi huyo
Ni msabili huyo ni mwindaji asie na silaha
Na usabili hauwezi
Hauwezi kutuletea ukombozi kamili wa jamii
Wala hauna lengo la mageuzi ya kimsingi
Kwani usabili ni usabili
Na mapinduzi ni mapinduzi
Na tunachokipambania katika nchi yetu
Kitakacholeta uhuru wa kweli
Siyo marekebisho
Ya mfumo wa ubepari-ukoloni-mamboleo
Bali ni mapindizi ya kisoshalisti
Ndiyo, sisi tunapigana
Kuung'oa kabisa na milele
Mfumo wote wa unyonyaji na udhalimu
Tunapambana
Kuuleta mfumo mpya kabisa
Mfumo wa usoshalisti
Tunafanya umoja na mshikamano
Kwa ajili ya mageuzi hasa
Na mageuzi hasa ni ukomunisti
Ndiyo kwa sababu
Sharti
Tujitolee mhanga
Kwa ujasiri na subira
Kufanya kazi ngumu
Lakini kazi muhimu
Kazi ya kujenga chama
Chama cha Wafanyikazi wa Kenya
CCW
CCW ni chama cha kikomunisti Kenya
CCW-kazi kwetu makomredi!…
Mwamko wa wafanyikazi wa Kenya unaongezeka
Hili tulilijadili kwa kirefu tulipoongea kwa simu dakika chache zilizopita.
Lakini kwa kuwa mambo yakiwekwa kwa maandishi yanaeleweka vizuri zaidi, nitachukua
nafasi hii kukariri kidogo yale tuliyoyajadili kufungamana na mada ya hapa
juu, CCW. Kama tulivyoshikilia siku nyingi, sasa wafanyikazi wa Kenya wanaendelea
kupata mwamko mpya kila siku. Wanazidi kuelewa, kwa uchungu wa kusalitiwa,
kwamba hawawezi kujikomboa ndani ya mfumo wa ubepari. Pia kila siku wanazidi
kutambua kuwa vyama vya kisiasa vinavyoongozwa na mabepari
na mabepari-uchwara
na vinavyoshikilia itikadi
za kibepari, haviwezi kuleta ukombozi wa wengi wanaonyonywa na kugandamizwa.
Wala hawawezi kukombolewa na harakati
za kidemokrasi zinazoongozwa na mabeberu kupitia kwa Mashirika Yasiyo
ya Serikali (NGO's)*.
Nani anaogopa ukomunisti Kenya?
Isitoshe, na muhimu zaidi, wanazidi kufahamu kuwa hakuna atakaekomboa
wafanyikazi ila muungano wao wenyewe na juhudi zao za mapambano. Aidha,
nimejifundisha, kwa kufanya kazi pamoja na wafanyikazi, kwamba hawana hofu
yoyote ya ukomunisti na mawazo ya kikomunisti. Hakika wafanyikazi wana kiu
kikubwa cha mawazo ya kimapinduzi, wanataka siasa zenye lengo la kung'oa
kabisa mfumo wa unyonyaji wa mtu kwa mtu. Na siasa zenye shabaha ya kung'oa
mizizi ya mfumo wa unyonyaji wa mtu kwa mtu si zingine bali ni za kisoshalisti.
Kutokana na hali ngumu ya maisha yanayozorota usiku na mchana, wafanyikazi
wanajua hawana chochote cha kupoteza kwa kuong'oa mfumo wa ubepari ukoloni-mamboleo.
Wale wanaoogopa ukomunisti ni mabepari na mabepari-uchwara.
Wakati mabepari-uchwara wanadai ati wakomunisti wasijitambulishe hadharani,
ati kutokana na propaganda zilizofanywa na maadui dhidi ya ukomunisti ati
Wakenya wanaogopa na kuchukia ukomunisti-wakati mabepari-mchwara wanadai
hivi, hakika wanadhihirisha hofu yao wenyewe inayotokana na siasa zao za kibepari-uchwara
za kuyumbayumba na za ubarakala. Kwani mabepari-uchwara, wenye kiburi cha
kudai kuzungumzia umma, wanaishi maisha ya kibepari-uchwara ya anasa na starehe
kutokana na uhusiano wao na ubepari na ukoloni-mamboleo. Hivyo, wanajua kuwa
wakijitokeza wazi na bayana kupambana dhidi ya ubepari na ubeberu watahatarisha
kazi zao, mapato yao na manono wanayokula kutoka kwa maadui hawa wa ukombozi
wa wengi wanaonyanyaswa nchini.
Mbinu mpya ya ubeberu: kuteka nyara harakati za kidemokrasi za
umma kupitia kwa Mashirika Yasiyo ya Serikali
Hivi sasa, wasabili (liberals) wengi ambao ni sehemu ya mabepari-uchwara,
hata wale waliyokuwa 'makomredi' wetu zama zile, wameajiriwa na Mashirika
Yasiyo ya Serikali yanayodhaminiwa na mabeberu au wasabili kutoka nchi za
Magharibi, wanafanya kazi ya kupigania marekebisho (reforms) ya mfumo unaotawala
nchi yetu. Lugha yao ni marekebisho wala si mageuzi, marekebisho ya kikatiba
na kidemokrasi wala si mageuzi ya kikatiba na kidemokrasi!
Ndiyo, kulingana na wasabili na mabepari-uchwara katika Mshirika Yasiyo
ya Serikali, Bunge, Mashirika ya Kidini, n.k., kushiriki kwao kwa harakati
za kidemokrasi (katiba mpya, haki za binadamu, n.k.) ni kazi (career). Na
waajiri wao, mashirika yenye uhusiano na wakoloni-mamboleo kwa njia moja
ama nyingine, ni wapinga-ukomunisti. Ndiyo kwa maana hivi sasa, harakati
za kidemokrasi Kenya zimetekwa nyara na nadharia za kidemokrasi za kibepari.
Mara nyingi, nimehudhria mikutano yao Ufungamano, Hilton Hotel, New Stanley
Hotel, Mt. Kenya Safari Club, Professional Centre, American Information Centre,
Safari Park Hotel, n.k., na kugundua haya yote. Utasikia wengi wakidai kadamnasi
ya wawakilishi wa mabalozi wa nchi za kibeberu ati ukomunisti ni udikteta
na ubepari ni sawa na demokrasi.
Kwa maoni ya wasabili na mabepari-uchwara wa Kenya, hasa waliyoko katika
Mashirika Yasiyo ya Serikali na Mashirika ya Kidini, Wakenya hawawezi kujikomboa
bila misaada ya mabeberu (wale wale wanaotunyonya). Kwao hata SAPs za Benki
ya Dunia na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ni nzuri kwa nchi yetu. Mabarakala
wanaodai kuwa katika msitari wa mbele wa harakati za kidemokrasi wanajitahidi
kuwadanganya wananchi kuwa mabeberu ni marafiki wa harakati za ukombozi za
Wakenya. Mwaka uliyopita huko Ufungamano, Nairobi, katika mkutano wa kuadhimisha
miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Ufafanuzi wa Haki za Binanamu wa Umoja wa
Mataifa, nilishuhudia Profesa Kivutha Kibwana akiupamba ubeberu kwa sifa
tilatila huku akisisitiza kuwa kitakachokomboa Kenya kutoka kwa udikteta
na umasikini ni Marekani tu! Ukisikiliza hotuba za viongozi hawa wa harakati
za kidemokrasi zinazoendelea, unaweza kupandwa na wazimu. Kwani, chambilecho
ndugu Mao Tse Tung, mabeberu ni marafiki wanaokuja kwa asali mdomoni na
mkuki moyoni!
Wanafanya maovu yaleyale wanayoyapinga!
Wote katika Mashiriki Yasiyo ya Serikali, ambayo yanachipuka kama vioga
kila siku, wanadai kutetea wanaonewa na kunyanyaswa, wote wanadai wanapigania
demokrasi na haki za binadamu, lakini harakati wanazoongoza zimefunikwa na
mwavuli wa ubeberu na itikadi ya kibepari. Si ajabu basi kuwa nimeshuhudia
kuwa Mashirika Yasiyo ya Serikali ni ngome ya ufisadi, ukabila, upendeleo
wa kikoo (nepotism), utapeli, ubarakala, unafiki, ulafi, usaliti na maovu
yote yale yanayofanywa na utawala wa imla wa Moi-Kanu. Ni kinyume kabisa
na matamko ya uwazi (transparency), utawala mzuri (good governance), demokrasi,
uaminifu, haki na maadali yote wanayohubiria serikali na umma. Si ajabu pia
kwamba wadhamini (mabeberu) wanamwaga mabilioni nchini kwa ajili ya Mshirika
Yasiyo ya Serikali. Si ajabu kwamba mabeberu wanapendelea Mashirika Yasiyo
ya Serikali kuliko vyama vya kisiasa ama serikali. Si ajabu kuwa Mashirika
Yasiyo ya Serikali-ambayo yamebaki kuwa Mashirika Yasiyo ya Serikali wala
siyo Mashirika ya Umma (civil society) yanajifanya kuwa yanawakilisha umma
(people driven this and people driven that, without even saying what they
mean by people). Si ajabu kwamba hakuna tofauti ya kimsingi kuhusu Katiba
Mpya kati ya Kamati ya Bunge inayoongozwa na Raila na ile ya Mashirika ya
Dini (na Mashirika Yasiyo ya Serikali): wote wanataka katiba mpya ya kitaifa
iwe ya kibepari tu, mfano wao (model) ni katiba za nchi za kibepari. Tofauti
kati yao ni njia ya kufikia katiba hiyo na nani atadhibiti mabilioni yaliyoahidiwa
na wafadhili kugharamia harakati za kikatiba.
Harakati za kikatiba-tofauti yetu na wasabili
Ndiyo kwa maana tumekuwa tukikariri, wakati wote katiba ni kioo cha hali
halisi ya maisha ya leo. Wakati wa ukoloni-mkongwe, katiba ya kitaifa ya
Kenya ilikuwa kioo cha kumulika hali na makinzano (contradictions) ya Kenya
chini ya ukoloni wa Waingereza. Katiba ilikuwa sehemu ya chombo cha dola la
kikoloni la kuhalalisha na kudumisha nyanyaso za wakoloni dhidi ya Wakenya.
Hivi leo Kenya iko chini ya ukoloni-mamboleo. Basi katiba ya kitaifa ambayo
wanapambana kuirekebisha (kumbuka wanasema kurekebisha wala siyo kugeuza)
ni kioo kinachomulika maisha ya leo ya Kenya chini ya udikteta na ukoloni-mamboleo.
Katiba ya leo inahalalisha unyonyaji wa mtu kwa mtu, imla, ubepari na ubeberu.
Na maadamu ukoloni-mamboleo hautang'olewa na kuja kwa katiba mpya, katiba
mpya itakayokuja, iwe kupitia kwa Kamati ya Raila au kwa Mashirika ya Kidini
na Mashirika Yasiyo ya Serikali, itaendelea kuwa nguzo ya kuulinda mfumo wa
ubepari-ukoloni-mamboleo, mfumo wa unyonyaji wa mtu kwa mtu. Hivyo basi, ni
uongo kudai kuwa katiba mpya italeta ukombozi wa kitaifa na wa wengi wanaonyonywa
na kugandamizwa. Isitoshe, tukitoboa ukweli wote, hapawezi kuwa na katiba
ya kitaifa katika taifa lililogawanyika kitabaka kama la Kenya.
Tunachosema badala yake ni kuwa katiba mpya inaweza tu kupanua uwanja wa
kuendeleza harakati za kitabaka ikiwa itaongeza demokrasi. Wafanyikazi na
umma kwa jumla hawatakombolewa na katiba mpya bali wanaweza kuitumia katiba
mpya kama ngazi ya kupandia kuelekea ukombozi wao, kuvunjiliwa kwa mfumo wa
ubepari na ukoloni-mamboleo. Tunaunga mkono harakati za kidemokrasi siyo kwa
sababu demokrasi itaondoa umaskini na kuleta ukombozi wa wengi wanaonyonywa
na kunyanyaswa, bali kwa kuwa demokrasi itatengeneza na kuboresha hali ya
kuoganaizi umma kupambana dhidi ya mfumo wa ubepari-ukoloni-mamboleo ambao
ndiyo msingi wa umaskini wa kunyonywa kwao. Demokrasi itasaidia wafanyikazi
na umma kuendeleza mapambano yenye shabaha ya kuleta usoshalisti ambao ndiyo
mfumo utakaoleta uhuru na ukombozi kamili wa wafanyikazi, jamii na taifa la
Kenya kwa ujumla. Wasabili, wanaoshikilia nadharia ya kibwanyenye ya demokrasi,
hawaelezi Wakenya ukweli huu kwa sababu ambazo hatuhitaji kuzieleza hapa.
Wala hawatupendi kwa kusema ukweli huu.
Basi pia si ajabu kuwa kila unapowatajia marafiki zetu wa zamani kuhusu
haja ya chama cha kikomunisti nchini Kenya wanaruka kwa ghadhabu, "Ati chama
cha kikomunisti! Hujui ukomunisti umeshaanguka? Ehhh hujui wafanyikazi wanaogopa
sana ukomunisti? Nani atadhamini chama cha kikomunisti?" Unajua, pale ubeberu
umefaulu zaidi katika sera zake za kuyateka nyara mapambano ya ukombozi ya
umma wa Kenya ni katika kuwafanya wengi (tangu mabepari-uchwara hadi hata
sehemu kubwa ya umma) ati hakuna chochote nchini kinachoweza kufanyika bila
misaada kutoka nje (kwa mabeberu). Hata wafanyikazi wenyewe hawawezi kujikomboa
bila misaada ya mabeberu. "Kwa hivyo, sharti wajitenge na siasa za kikomunisti
ili kupata misaada ya kudhamini harakati zao."
Mara nyingine utawasikia wakisema kuwa wamechoka na vyama vya kisiasa.
Ati vyama vya kisiasa vimewasaliti watu mara nyingi hata wananchi leo hawana
imani navyo. Utawasikia wakizungumzia 'tabaka la wanasiasa' (political class).
Ati tabaka la wanasiasa ndilo limekuwa likivuruga harakati za kidemokrasi
kwa kuwasaliti wananchi wanaopigania katiba mpya. "Tutahadhari na tabaka la
wanasiasa. Tabaka la wanasiasa ni la vibarakala. Watakaoleta mabadiliko ya
kikatiba na hatimaye ukombozi wa kitaifa ni Mashirika Yasiyo ya Serikali.
Tunapigania katiba itakayoendeshwa na watu (people driven constitution)."
Hii ndiyo lugha ya NCE (kina Profesa Kivutha Kibwana, Willy Mutunga, Davinda
Lamba, Kepta Wendati, Timothy Njoya, Mashirika ya Kidini, n.k. Lakini
hata kama vyama vya kisiasa vimesaliti watu kwa njia moja ama nyingine, hii
ni sababu ya kutosha kusema havihitajiki? Kunaweza kuwa na mabadiliko ya kisiasa
bila vyma vya kisiasa? Kuna kitu kama 'tabaka la wanasiasa'? Sisi tunajua
kuwa tabaka ni kundi kubwa la watu ambalo lina mahusiano maalumu na njia
za uzalishaji mali. Kwa mfano, kuna tabaka la mabepari ambalo linamiliki viwanda,
mashini, malighafi na hivyo utajiri na uwezo wa kunyonya wafanyikazi. Kwa
upande mwingine, tabaka la wafanyikazi linalazimika kuishi kwa kuuza nguvukazi
(kwa kunyonywa) kwa kuwa halina umilikaji wa viwanda, mashini, malighafi,
n.k. Unawezaje kuzungumzia katiba inayoendeshwa na watu katika nchi iliyogawanyika
kitabaka kama Kenya. 'Watu' ni nani katika muktadha huu? Ni wazi kuwa wasabili
wa Kenya wanaparaganya maneno ili kuwarubuni umma kwa masilahi yao ya ubarakala.
Mara utawasikia wakisema ati walikuwa kwa harakati za kimapinduzi zama
hizo lakini hatukufika popote kwa sababu ya fulani au kwa sababu hii au ile.
Ati makosa makubwa yalifanyika na kuleta hasara kubwa ya watu kufungwa, kuwauwa,
kuwa wakimbizi na kutawanyika. Ndiyo, makosa yanaweza kuwa yalifanyika, lakini
hii ina maana kuwa hatuwezi kujifunza kutokana na makosa hayo na kuanza
upya? Tukaae tu tusifanye chochote kwa kuogopa kufanya makosa? Si yule ambae
hafanyi makosa ni yule ambae hafanyi chochote? Nadharia ya kikomunisti ya
elimu inatufundisha kuwa kufanya kunaleta kujifunza. Kadiri tunavyoshiriki
katika kazi halisi ya kujenga chama ndipo tunapata maarifa zaidi ya kujenga
chama. Na mara nyingi tunapata maarifa hayo baada ya kufanya makosa na kuyarekebisha.
Kwa muhtasari, siasa za kukosoa wanaojaribu bila kujaribu ni siasa sumu za
kuvunja mioyo ya wanaojaribu. Wakati umefika wa kujitenga kabisa na siasa
hizi za kibepari-uchwara na kujasiri kufanya kazi ya kujenga chama cha aina
mpya, chama cha kikomunisti.
Haja ya Chama cha Kikomunisti
Kwa ufupi, ninachojaribu kukisema hapa ni kwamba kuna haja kubwa mno ya
chama cha kikomunisti nchini. Na kuwepo kwa chama cha kikomunisti ni kupambana
siyo tu dhidi ya ubepari wa ndani na nje unaodhibitiwa na dola la imla la
Moi-Kanu, bali vilevile ni kupambana dhidi ya wasabili na mabepari-mchwara
na kazi kubwa wanayofanya ya kupotosha lengo la hatimaye la uhuru wa kitaifa
na ukombozi wa wengi wanaonyonywa na kugandamizwa.
Kuna haja kubwa ya chama cha kikomunisti Kenya kwa kuwa bado hakipo! Ni
jukumu letu la kihistoria, kama wakereketwa wa ukomunisti kufanya kazi ya
kuanza kukijenga. Tayari tumechelewa lakini wahenga walisema afadhali kuchelewa
kuliko kutofika.
Kuna haja ya chama cha kikomunisti kwa kuwa ni harakati za kimapinduzi
tu ambazo zitaleta mabadiliko ya kimsingi nchini. Na waanzilishi wa ukomunisti
wa kisayansi walisisitiza, bila nadharia ya kimapinduzi hapawezi kuwepo harakati
za kimapinduzi. Na hadi wa leo hakuna nadharia ya kimapinduzi zaidi kuliko
nadharia ya kikomunisti. Aidha, Karl Marx alilisisitiza, mawazo ya kimapinduzi
huwa nguvu za kimapinduzi yanapowafikia umma. Kwani lengo la hatimaye la
falsafa ya kimapinduzi siyo kuitafsiri dunia bali kuibadilisha. Basi tunahitaji
chombo cha kuwasilisha mawazo ya kimapinduzi, ukomunisti, kwa wafanyikazi.
Chombo hicho ni chama cha kikomunisti.
Historia ya Kenya, na zaidi ya leo, inadhihirisha harakati za kitabaka
wazi na bayana. Harakati za kitabaka kati ya waajiri na waajiriwa, wafanyakazi
na mabepari, matajiri na maskini, mijini na mashambani, yanajidhihirisha
kwa namna mbali mbali, migomo ya wafanyikazi, mapambano ya kudai ardhi, mapambano
ya wakulima wadogo wa majani-chai, kahawa, mchele, miwa, n.k. dhidi ya serikali
na vyama vya ushirika vinavyoongozwa na wanyonyaji, maandamano ya wanafunzi,
vita kati ya mabaraza ya miji na wachuuzi, harakati za kudai demokrasi, haki
za binadamu na katiba mpya, unyama wa polisi dhidi ya raia, uhalifu, n.k.
Hakuna mtu yoyote anaeelewa hali halisi ya nchi yetu ambae anaweza kukanusha
kuwepo kwa harakati za kitabaka ambazo haziwezi kuepukika katika nchi iliyogawanyika
kitabaka kama Kenya.
Kuna haja ya kuwa na chombo cha kuchochea harakati za kitabaka, kuwafanya
wanaonyonywa kuchukia wanyonyaji wao, wanaodhulumiwa kupambana dhidi ya wadhalimu
wao. Kuna haja ya kuwa na chombo cha kusambaza ukweli nchini kuwa hapawezi
kuwa na usawa kati ya matajiri na maskini. Wala mwaajiri na mwaajiriwa hawawezi
kuwa na uhuru, demokrasi na utekelezwaji wa haki za binadamu sawa hata kuwepo
na katiba ya aina gani. Kuna haja ya chombo cha kufichua ukweli kuwa u-Moi
bila Moi ni sawa na u-Moi na Moi. Kuna haja ya kuwepo na chombo cha kuendelea
kuwahakikishia wafanyakazi kuwa hawawezi kujikomboa ndani ya mfumo wa ubepari/ubeberu,
mfumo unaopalalia na kutia mbolea unyonyaji wa mtu kwa mtu. Kuna haja ya
kuwa na chombo cha kuwakumbusha wafanyikazi na umma unaonyonywa kuwa hawawezi
kukombolewa na mtu yoyote yule ila muungano wao na mapambano yao ya kufa
na kupona. Kuna haja ya kuwa na chombo cha kubeba tochi ya kiitikadi ya kumulika
barabara sahihi ya mapambano ya ukombozi wa wafanyikazi na wote wanaonyonywa.
Kuna haja ya kuwepo na chombo cha kufafanua kwa maneno na vitendo kuwa ukombozi
kamili wa wafanyikazi utaletwa na mapinduzi ya kikomunisti ambako tabaka
la wafanyikazi litanyakuwa na kudhibiti nguvu za dola kutoka kwa tabaka linalotawala
sasa, tabaka la mabepari na vibaraka wa mabeberu. Tuna haja ya chombo cha
kuwafundisha wafanyikazi mbinu na hali za kuzatiti na kufanya mapinduzi
ya kisoshalisti. Chombo hicho, bila shaka, ni chama cha aina mpya tofauti
na vyama vilivyopo sasa, chama cha kikomunisti.
Taifa letu liko chini ya himaya ya ubeberu kwa sura ya ukoloni-mamboleo.
Hatuko huru kama taifa. Ndiyo kwa maana tunatawalwa kiuchumi, kisiasa, kitamaduni
na hata kijeshi na ubeberu wa kimataifa. Chambilecho Julius Kambarage Nyerere,
kutawalwa kwa vyovyote vile ni vibaya, bali kutawalwa kimawazo ni vibaya
mno. Bali Wakenya tunatawalwa kimawazo na mabeberu. Elimu inayofundishwa shuleni
na vyuoni nchini ni ya kusambaza itikadi ya kibepari na kibeberu. Vyombo
vya habari, redio, televisheni na magazeti ni za kusambaza itikadi za kibepari
zinazofundisha uongo ati mfumo wa ubepari, wa unyonyaji wa mtu kwa mtu, ati
ni mfumo wa haki na wa kimaendeleo, ni mfumo usiyoweza kuepukika. Usiku na
mchana Wakenya wanapigwa propaganda ati ukomunisti ni mfumo mwovu na wa kupinga
maendeleo. Tangu kuanguka kwa dola za kuparaganya ukomunisti (revisionist
regimes) za Usovieti (Urusi) na Ulaya Magharibi, mabeberu wamezidisha kiburi
cha kusifu uwezo wa ubepari na ubeberu dhidi ya ukomunisti, kiburi cha kudai
ati hapawezi kuwa na maisha mengine bora duniani isipokuwa yale ya ubepari
na ubeberu.
Bila ukomunisti maisha ni magumu mno kwa umma wa mataifa yaliyokuwa
ya Usoviet na Ulaya Mashariki
Wala Wakenya hawaelezwi kuwa kuanguka kwa dola za kuparaganya ukomunisti
duniani kumedhihirisha hata zaidi kuwa ubepari na ubeberu ni adui mkubwa
wa wafanyikazi na umma kwa ujumla. Hawaambiwi kuwa hivi leo Urusi, Ulaya Mashariki
na nchi zilizokuwa za Kisovieti zinaongozwa na udikteta wa mafia na vibaraka
wa mabeberu. Mali ya umma inaporwa na kupewa watu binafsi na mabepari wa
kigeni kwa jina la ubinafsishaji. Ubeberu umefunguliwa milango kubakua rasilimali
za mataifa haya vururumtende. Nchi hizi zimepoteza uhuru wao wa kitaifa na
zimefanywa kutegemea misaada na mikopo kama mataifa mengine yaliyoko chini
ya ukoloni-mamboleo. Pengo kati ya matajiri na maskini limeongezeka mno.
Ufukara kwa wengi, njaa, maradhi, ghasia, vita vya kikabila, ufisadi, uhalifu
wa kila aina, ubaguzi wa rangi, umalaya, matumizi ya madawa ya kulevya, kilio
cha wengi- haya yote yameibuka na yanaongezeka usiku na mchana. Ufanisi wote
uliyofanywa na mataifa haya katika nyanja za elimu, sayansi, tekinolojia na
adili za kiutu hivi leo yameporomoka. Vyombo vya dola na vya kusambaza habari
vimetangaza vita vya kiitikadi dhidi ya umma wa Urusi, Ulaya Mashariki na
mataifa yaliyokuwa ya Kisovieti, vinavuruga utamaduni wao na kuparaganya historia
ya kimaendeleo yao ya kimaendeleo. Na huku Kenya wananchi wanadanganywa ati
watu wa mataifa haya wanafurahia demokrasi na haki za binadamu. Kuna haja
ya chombo cha kukanusha uongo huu na kueleza umma wa Kenya. Chombo hicho ni
chama cha kikomunisti.
Wala hawaelezwi kuwa hivi leo ubeberu umekuwa huru mno kuyanyonya na kuyafukarisha
mataifa ya Afrika, Amerika ya Kusini na Asia kuliko wakati kulipokuwa na
Usoviet na ukuta wa Berlin. Mashirika ya kibepari yanazidi kutawala uchumi
wa dunia. Wakati nchi za kibeberu zinazidi kurundika utajiri, nchi zilizoko
chini ya ubeberu zinadidimia kwa lindi la umaskini usiku na mchana. Ndani
ya nchi za kibeberu zenyewe, pengo kati ya matajiri na maskini linazidi kupanuka.
Jamaa chache tajiri zinatawala uchumi wa dunia. Mashirika ya mabeberu ya
kuimarisha uchumi wa kikoloni-mamboleo duniani kama Shirika la Biashara la
Dunia (WTO), Mikataba ya Kimataifa Kuhusu Vitega Uchumi (MAI), Benki ya Dunia,
Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) yanafanya kazi ya kuondoa ufanisi wowote
ule uliyofanywa na nchi za 'dunia ya tatu' katika viwanda, biashara, kilimo,
elimu, afya, n.k. Kwa jina la uduniishaji (globalisation) ubeberu umejipatia
haki ya kupora rasilimali za kimaumbile na za watu za mataifa yaliyoko chini
ya ubeberu kama Kenya. Matokeo yake ni kwamba wakati kumekuwa na ufanisi mkubwa
ajabu katika sayansi na tekinolojia, Wakenya bado wanalima kwa jembe na panga,
wanakufa kwa njaa na maradhai yanayoweza kutibika, wanapika kwa kuni, wanaishi
maisha ya umaskini na ushenzi. Kuna haja ya chombo cha kuchambua athari za
kuvunjika kwa Usoviet na kuongezeka kwa unyama wa ubeberu ulimwenguni. Chombo
hicho ni chama cha kikomunisti.
Kilichoanguka si ukomunisti bali ni dola za waparaganyaji wa ukomunisti
Baada ya mapinduzi ya Oktoba, 1917, huko Urusi kulitokea nguvu
za dola za kuupinga ubeberu ambao kabla ya hapo ulikuwa ukinyanyasa ulimwengu
vururumtende. Wanaonyonywa na kugandamizwa ulimwenguni wakawa wamepata dola
la kupigania, kutetea na kuhami masilahi yao ya uhuru. Ubeberu ukapigwa breki
na mataifa yaliyokuwa chini ya ukoloni duniani, kama Kenya, yakaanza kujikomboa
moja baada ya lingine hadi ukoloni-mkongwe ukakaribia kuondolewa kabisa
duniani. Harakati za kitabaka ndani ya mataifa mbali mbali zikachacha na
kuona matumaini upande wa wengi wanaopigania jamii ya usawa na utu. Ukomunisti
ukawa si nadharia tu bali mfumo halisi wa kijamii-kiuchumi uliyokuwapo duniani.
Kutokana na ufanisi wa usoshalisti huko Usovieti, mataifa ya Ulaya Mashariki
kama Ujerumani Mashariki, Poland, Bulgaria, Czekoslovakia, Rumania, Hungary
na Albania wakafaulu kufanya mapinduzi ya kisoshalisti pia baada ya vita
vya pili vya dunia. Mapinduzi ya kisoshalisti huko Uchina mnamo mwaka wa
1949, na baadae huko Korea Kaskazini, Cuba na Vietinum yakaongeza dola na
mataifa ya kikomunisti duniani. Harakati za kitabaka za kimataifa zikadhihirika
wazi zaidi, kwa upande mmoja wa kupinga maendeleo ni ubeberu wa kimataifa
ukiongozwa na Marekani na kwa upande mwingine wa kupigania maendeleo ni usoshalisti
wa kimataifa ukiongozwa na Urusi. Shabaha ya ubeberu wa kimataifa ni kudumisha
ubepari na ubeberu ulimwenguni ambapo lengo la usoshalisti wa kimataifa
ni kupinga ubepari na ubeberu ulimwenguni.
Lakini kuanzia mwaka wa 1956 (party congress under Khrushchev), baada
ya kifo cha Joseph Stalin (1953 Stalin alikufa), kiongozi wa Usovieti na
Chama cha Kikomunisti cha nchi hiyo, na mtu mashuhuri katika ukomunisti
wa kimataifa, uongozi wa dola la Usovieti, Chama cha Kikomunisti cha Kisovieti
na ukomunisti wa kimataifa ukachukuliwa na waparaganyaji (revisionist).
Waparaganyaji wakaanza kuuharibu ukomunisti kwa kuupindua kutoka kwa misingi
yake na kuuelekeza kwa barabara ya ubepari asteaste. Walianza njama zao za
kuuharibu ukomunisti kwa kulipaka matope jina la Stalin na kwa kufanya hivyo
la Vladmir Lenin, alieongoza mapinduzi ya kwanza ya kisoshalisti duniani.
Udikteta wa wafanyikazi ambao ndiyo nguzo ya kujenga jamii ya usoshalisti
ukaondolewa polepole na nafasi yake kuchukuliwa na 'dola la watu wote', ambalo
kwa kweli lilikuwa ni dola la kupanda mbegu za kurudisha mabepari wapya
Usovieti na Ulaya Mashariki. Ili kufanya hivyo, kina Khrushchev, Breznev
na hatimaye Gorbachev wakatunga nadharia ya kuparaganya ukomunisti ya kudai
ati matabaka hayakuwepo tena Usoviet na Ulaya Mashariki ati kilichobaki tu
ati ni makinanzano baina ya watu. Wakati wote huu, viongozi wa dola na wasomi
wakawa wanatumia vyeo vyao kuishi maisha ya anasa na starehe zilizokuwa mbali
na umma. Na ili kulipia anasa na starehe zao wakawa wanafanya njama za kupora
mashirika ya umma. Mashirika ya umma yakawa kama mali binafsi ya viongozi
wa dola, jama na marafiki zao pamoja na vibaraka wao waliofanywa mameneja
wa kuyasimamia. Badala ya uwezo wa wafanyikazi wa kudhibiti mashirika ya
umma kuongezeka ukawa unapungua.
Badala ya makucha ya kiitikadi na kiuchumi ya wapinga mapinduzi kukatwa
yakazidi kuwachwa kuendelea kumea. Uchumi wa viwanda na kilimo ukazidi kuelekezwa
kuwa wa ubepari kwa kisingizio kimoja ama kingine. Kwa kisingizio cha kuongeza
uzalishaji mali, mali ya binafsi ikaruhusiwa na watu binafsi waliokuwa na
uhusiano na uongozi wakaruhusiwa kufanya biashara na kuajiri wafanyikazi.
Uchumi wa kisoshalisti ukawa unahujumiwa. Bidhaa kutoka mashirika ya umma
zikawa zinauzwa kwa makampuni ya watu binafsi kwa bei rahisi mno na baadae
kuuziwa wananchi kwa bei ghali na hivyo kuwazalishia mabepari faida kubwa.
Badala ya kutekeleza mipango ya kiuchumi ya usoshalisti ya kutosheleza mahitaji
ya jamii, dola la Usoviet likaelekeza uzalishaji kuingia katika mtego wa
ubeberu wa kutumia rasilmali nyingi mno ketengeneza na kulimbikiza silaha.
Badala ya kuzidisha harakati za kitabaka dhidi ya ubeberu wa kimataifa, waparaganyaji
wa Usoviet na Ulaya Mashariki, wakawa wanafanya juhudi za kuzipoza kwa kuhubiri
kuhusu kuishi kwa amani kati ya mataifa ya kisoshalisti na ya kibeberu. Wakawa
wanazungumzia kuhusu kuwepo kwa mambo ya ubinadamu yaliyoko juu ya mipaka
ya kitabaka.
Wakati huo huo waparaganyaji wakawa wanafanya matamshi na vitendo vya
kupinga haki ya watu wa mataifa yaliyoko chini ya ubeberu kupigania ukombozi
wao kutoka kwa ubeberu. Kwa tangu mwaka wa 1956 hadi mwaka wa 1988, uparaganyaji
ulikuwa unaguguna ukomunisti huko Usoviet na Ulaya Mashariki. Uparaganyaji
wa ukomunisti una maana kuwa vyama vya kikomunisti huko Usoviet na Ulaya Mashariki
vilikuwa vinaurudisha ubepari. Kazi hii ya kuurudisha ubepari ilikamilishwa
na Mikhael Gobachev na nadharia yake ya glasnost na perestroika ambayo ilifanya
mapinduzi ya kibepari na kuwarudishia mabepari nguvu za dola, kiuchumi na
kisiasa chini ya Boris Yeltsin. Hivyo basi, ni vyama vya uparaganyaji vilivyoanguka
Urusi, mataifa yaliyokuwa ya Usoviet, Ulaya Mashariki na kwingineko duniani
wala si ukomunisti. Si ukomunisti uliyovunjika bali ni dola za uparaganyaji
wa ukomunisti zilizosambaratika. Kenya tunahitaji chombo cha kueleza historia
ya kweli ya ukomunisti na kupinga propaganda za kihasama za mabeberu na vibaraka
wake dhidi ya ukomunisti. Tunahitaji chombo kinachoweza kutufundisha kutoka
kwa historia ya dunia kuhusu kila inatupasa kukifanya na kile inatupasa kukiepuka
kukifanya. Chombo hicho ni chama cha kikomunisti.
Kuvunjika kwa koleo si mwisho wa uhunzi
Harakati za kitabaka zinaendelea kote duniani, wala haziwezi kuepukika
kadiri kuna mifumo ya kitabaka. Ndani ya mataifa ya kibepari au kibepari-kikoloni-mamboleo
kama Kenya, mapambano yanaendelea kila siku, mapambano kati ya mabepari na
wafanyikazi, waajiri na waajiriwa, matajiri na maskini, wachache wenye kumiliki
wenye kumiliki kiasi kikubwa zaidi cha rasilimali za kitaifa na wengi walioporwa
haki ya kufurahia rasilimali za kitaifa. Kimataifa mapambano yanaendelea
kila siku kati ya ubeberu wa kimataifa unaopigania kutawala ulimwengu na
usoshalisti wa kimataifa unaopinga ubeberu, kati ya nchi za kibeberu na nchi
zilizoko chini ya ubeberu, kati ya mashirika ya kibepari (multinationals)
yanayodhibiti uchumi wa kimataifa kwa kisingizio cha uduniishaji (globolisation)
na masoko huria (free markets), ubinafsishaji (privatisation) kwa upande mmoja
na mataifa yaliyoko chini ya ukoloni-mamboleo huu na umma wa mataifa ya kibepari
kwa upande mwingine. Harakati za kitabaka zinaendelea na kudhihirika kwa
njia mbalimbali, kisiasa, kiuchumi, kitamaduni, kiitikadi na kijeshi.
Kila pahali duniani, mkiwemo Urusi, nchi zilizokuwa chini ya Usovieti,
Ulaya Mshariki, wakomunisti wako katika msitari wa mbele wa harakati za kupinga
ubepari, ubeberu na kukomboa nchi zao na dunia kutoka kwa mfumo wa unyonyaji
wa mtu kwa mtu na kuleta usoshalisti badala yake. Vyama vya kikomunisti
vinazatiti mapambano ya wafanyikazi na umma usiku na mchana. Ni muhimu tutekeleze
jukumu letu la kimataifa kwa kuanzisha na kujenga chama cha kikomunisti
Kenya ili tuwe sehemu ya ukomunisti wa kimataifa.
Tujifunze kutoka kwa historia yetu
Swala kuhusu haja ya chama cha kikomunisti si swala la mjadala kati yetu
wakomunisti. Kilihitajika tangu zamani. Kingelikuwako chama cha kikomunisti
nchini Kenya hakika tungelikuwa mbali sana kimaendeleo kama taifa. Tungelikuwa
tunajiunga na chama ambacho tayari kipo. Wala hatungelikuwa na jukumu la
kukianzisha. Kwa sababu hii, swala la kimsingi linalotukabili ni jinsi ya
kuanzisha chama chenyewe. Na swala hili halitasuluhishwa kinadharia tu lakini
hasa kimatendo. Tunapoanza kazi halisi ya kujenga chama chenyewe ndipo tutakapoongeza
ujuzi wetu wa kukijenga.
Historia ya Kenya, hasa kati ya 1979 na 1992, ya kupinga udikteta na ubeberu
inaonyesha kuwa kulikuwa na vyama vingi vya chini kwa chini ambavyo vilikuwa
vinajitambulisha na usoshalisti. Hakika sijui chama chochote cha chini kwa
chini ambacho hakikudai kuwa cha mlengo wa kushoto na kuunga mkono harakati
za kisoshalisti. Lakini vyama hivi havikudumu. Vilikuwa vinaibuka na kufa.
Ndiyo kwa maana, ingawa vilichangia sana katika kuleta mfumo wa vyama vingi,
hivi leo havipo, Aidha, athari za siasa za kisoshalisti ni haba mno. Moja
wapo wa sababu ya kutokua kwa vyama vya kisoshalisti vya enzi hizo ni kuwa
ingawa programu na katiba zao zilivitangaza kuwa vyama vya wafanyikazi havikuwa
na wafanyikazi. Wala hapakuwa na juhudi halisi za kuwaingiza wafanyikazi
kwa vyama hivi na kuwafanya wachukue madaraka ya kuendesha vyama hivi. Vyama
hivi vilikuwa vya mabepari-uchwara: hasa walimu na wanafunzi wa chuo kikuu.
Makinzano ya ubepari-uchwara ya usabili (liberalism), ubarakala (oportunism)
na uanakisti ukazuia vyama hivyo kukua na kudumu. Tunajifunza nini kutoka
hili? Chama cha wafanyikazi lazima kiwe chama cha wafanyikazi kwa maneno na
kwa vitendo. Wafanyikazi wapo Kenya, mijini na mashambani. Sharti tufanye
juhudi za maksudi kabisa za kuwafikia na kuwaingiza katika harakati za kujenga
chama chao, chama cha kikomunisti. Tukiazimia na kutekeleza shabaha hii tutaweka
msingi wa kudumu wa chama cha kikomunisti cha Kenya.
Chama cha Wafanyikazi cha Kenya (CCW) ni chama cha kikomunisti. Lengo
la hatimaye la CCW ni kuongoza wafanyikazi wa Kenya kuangusha mfumo wa kinyama
na wa kupinga maendeleo, ubepari na ubeberu, na badala yake kujenga mfumo
wa kimaendeleo na kiutu, mfumo wa usoshalisti. Yaani shabaha ya CCW ni kuvunjilia
mbali na milele mfumo wa unyonyaji wa mtu kwa mtu. Kwa maneno mengine, CCW
ni chama cha kuonyesha njia ya ukombozi kamili wa wafanyikazi, wakulima masikini
na wote wanaonyonywa na kugandamizwa. Kwani njia ya ukombozi kamili wa wanaonyonywa
na kugandamizwa ni njia ya kimapinduzi, mapinduzi ya kisoshalisti.
Nduguye
Sunday, 13 February 2000
Glossery:
Kiswahili-English
Published by Kenya Socialist Democratic Alliance
(KSDA)
email: harakatips@hotmail.com
Home